Fuso latumbukia mto Kilombero
Lori aina ya fuso lenye namba za usajili T 139 AEM, likiwa na shehena ya magunia ya mpunga, limetumbukia kwenye mto Kilombero uliopo mkoani Morogoro mapema asubuhi ya leo Ijumaa Julai 14, baada ya kupitiliza kwenye kivuko kinachotumika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Azam TV, Robert Mayungu aliyepo mkoani Morogoro, gari hilo lilikuwa linatokea Ulanga kuelekea Ifakara ambako ndiyo makao makuu ya wilaya hiyo.
Juhudi mbalimbali zimefanyika katika kulinasua gari hilo ambalo lilikuwa limepinduka na matairi yake kuwa juu, zilizoongozwa na wananchi wa kawaida.
Jitihada hizo zilizaa matunda na kufanikiwa kuligeuza japo kwa kiasi fulani lori hilo lililoonekana kuharibika huku kioo chake cha mbele kikiwa kimevunjika vibaya.
Hakuna taarifa yoyote ya vifo au majeruhi yaliyosababishwa na ajali hiyo, kwani dereva wake ambaye hakukufahamika mara moja, aliweza kuruka na kujiokoa.