news

Azam yaiduwaza Yanga Taifa

TIMU ya Azam FC jana ilifanikiwa kuibuka bingwa wa mchezo wa Ngao ya Jamii unaoashiria kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuifunga Yanga mabao 4-1 kwa mikwaju ya penalti, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Penalti hizo ziliamua mshindi wa mchezo huo, baada ya sare ya mabao 2-2 katika muda wa dakika 90.
Mabao ya penalti ya Azam yalifungwa na Shomari Kapombe, Himid Mao, John Boko na Michael Bolou, huku ya Yanga moja ilifungwa na Deugratius Munishi ‘Dida’, huku waliokosa ni Hassan Kessy na Haruna Niyonzima.

Yanga ndio waliokua wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 20 kipindi cha kwanza cha mchezo kwa penalti mfungaji akiwa mshambuliaji, Donald Ngoma, baada ya David Mwantika kumfanyia madhambi Ngoma akiwa eneo la hatari na mwamuzi Ngole Mwangole kuamuru penalti hiyo.

Dakika mbili baada ya bao hilo, Ngoma aliwanyanyua tena mashabiki wa Yanga vitini akiandika bao la pili, akimalizia pasi safi ya Amissi Tambwe. Azam FC ilizinduka dakika 26, almanusura Kapombe aipatie bao lakini alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 na mpira kutoka nje.

Licha ya kupambana ili kusawazisha mabao hayo, Azam ilishindwa kufurukuta na kushuhudia ikimaliza kipindi cha kwanza ikiwa nyuma kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili kilianza kwa Kapombe kukosa bao dakika ya 65, baada ya kupiga mpira kwa kichwa akiwa ndani ya 18 na kutoka nje.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Azam ikipiga hesabu ni vipi itaweza kujinasua katika kutia aibu mashabiki wake waliojitokeza uwanjani kuishangilia.

Hata hivyo, dakika ya 74, Kapombe aliweza kuisaidia timu yake kupata bao baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jean Mugiraneza ‘Migi’.
Bao hilo liliibua matumaini mapya kwa Azam, ambayo ilipigana hadi kufikia dakika ya 90 walipoandika bao la pili na kusawazisha kwa mkwaju wa penalti, uliopigwa na John Bocco baada ya beki wa Yanga, Vicent Bossou, kushika mpira akiwa ndani ya 18.

Timu hizo zilimaliza dakika tisini zikiwa sare ya bao 2-2, hali iliyowaacha mashabiki wa Yanga waliofurika uwanjani hapo midomo wazi wasiamini kilichotokea.

Mchezo huo wa ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu, ulikuwa na hamasa kubwa hasa kwa timu ya Azam FC ambayo ilikuwa ikitambulisha kikosi chake cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu ujio wa kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Mhispania, Zeben Hernandez.

Yanga: Deogratius Munishi “Dida”, Hassan Kessy, Haji Mwinyi, Mbuyu Twite, Vicent Bossou, Said Juma, Thaban Kamusoko, Amissi Tambwe/ Simon Msuva, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Juma Mahadhi/Malimi Busungu.

Azam: Aishi Manula, Ismail Adam, Bruce Kagwa, David Mwantika, Himid Mao, Jean Muguraneza, Shomari Kapombe, Salum Aboubakar, John Bocco, Shaban Chilunda/ Francisco Zekumbariwa na Ramadhani Singano/Mudathiri Yahaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *