news

Bakhresa azidi kupaisha sekta ya viwanda

KAMPUNI ya Bakhresa Foods imedhamiria kuongeza viwanda vingine vya usindikaji matunda hapa nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima.

Ahadi hiyo imetolewa juzi Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Said Bakhresa, katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, jijini Dar es Salaam.

Bakhresa alisema wana mpango wa kujenga kiwanda kimoja kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwamba wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda hadi Dar es Salaam ndipo wayauze.

“Kuanzia Oktoba 15, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani na kwa siku tunapata semi trela zaidi ya 30. Yakimalizika ya kule tunaanza kupokea mengine kutoka mikoa ya Pwani na Kusini.

“Tukijenga kiwanda Kanda ya Ziwa, tutapunguza adha ya wadau kusafirisha matunda kutoka kule hadi hapa kiwandani na badala yake sisi tutakuwa tunasafirisha concentrated juice na kuileta hapa kwa hatua zaidi za usindikaji,” alisema bilionea huyo.

Pamoja na hali hiyo, alisema ni muhimu kuwa na viwanda vya vyakula vya nafaka kwenye mikoa ya Kusini na kwamba hadi sasa wameajiri wafanyakazi zaidi ya 8,000 wakiwemo Watanzania 180 ambao wameajiriwa kwenye matawi yake nje ya nchi.

“Hawa tunawalipa kama expatriates,” alisema.

Alisema hivi sasa kampuni yake imeshafungua matawi mengine kwenye nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Kampuni ya Bakhresa Foods inatengeneza vyakula mbalimbali zikiwemo juisi, soda, maji, biskuti, ice-cream, vyakula vya nafaka kama ngano, mahindi, mchele na bidhaa za kuokwa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimhakikishia Bakhresa nia ya Serikali ya awamu ya tano kushirikiana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwani imedhamiria kukuza uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji wa viwandani.

“Serikali inathamini mchango wa wenye viwanda katika nchi yetu. Tunawashukuru ninyi ambao ni wakongwe kwenye sekta hii na kwa hiyo tunawaomba msikate tamaa, muendelee kufungua viwanda zaidi ili wananchi wetu wapate mahali pa kuuzia mazao au bidhaa zao,” alisema Majaliwa.

Licha ya hilo, alimwomba Bakhresa aangalie maeneo mengine zaidi ya kuwekeza kama vile sekta za hoteli na utalii ili kusaidiana na Serikali kukuza uchumi wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *